WATUMISHI MPRU WASHIRIKI MKUTANO WA OACPS 24
WATUMISHI MPRU WASHIRIKI MKUTANO WA OACPS 24

Alhamisi, 12 Septemba 2024, Dar es Salaam

Watumishi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) wameshiriki Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (OACPS) wanaoshughulikia sekta ya uvuvi na mifugo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam,  Septemba 11, 2024.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.

Akizungumza alipokuwa akihutubia katika mkutano huo, Waziri Majaliwa alisema serikali ya awamu ya sita ipo katika harakati ya kukuza Uchumi wa Buluu kwani sekta ya uvuvi kwa sasa inaingiza mapato ya shilingi trilioni 2.94 kwa mwaka, na sekta inakua kwa wastani wa asilimia 1.9 kwa mwaka.

Aidha, Majaliwa aliwataka mawaziri hao kuendelea kudumisha mshikamano wa nchi wanachama, kuimarisha na Kuhifadhi mazingira ya bahari, mito na maziwa, kuandaa utaratibu wa pamoja wa kuwekeza katika tafiti za kisayansi na kiteknolojia, kukuza wigo wa ushirikiano wa wadau wa kimataifa pamoja na kujiunganisha na taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo ili kurahisisha upatikanaji wa rasilimali fedha.

Naye kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiwasilisha taarifa ya utangulizi kuhusu yale yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo amesema mkutano huo utaangazia changamoto zinazotishia ustawi wa Rasilimali za Bahari na uvuvi ikiwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi na uvunaji uliopitiliza.

Kaimu Meneja wa MPRU, Bw. Davis Mpotwa alishiriki mkutano huo wa Mawaziri wa Umoja wa Nchi za Afrika, Carribean na Pacific (OACPS).