OFISI YA MKUU WA MKOA NA TAASISI ZINGINE ZATAKIWA KUSHIRIKIANA KATIKA KULINDA MAENEO YA HIFADHI ZA BAHARI NA RASILIMALI ZAKE
Jumanne, 3 Septemba 2024, Mtwara
Afisa Tawala Mkuu, Bw. Deodat Mmanda ametoa rai kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Taasisi nyingine kushirkiana kikamilifu kuyalinda Maeneo ya Hifadhi sambamba na rasilimali zinazopatikana ikiwa ni pamoja na utalii.
Ametoa rai hiyo alipokuwa akihutubia kwa wananchi wa Mtwara akimwalikilisha Kaimu Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) wakati wa mwendelezo wa Tamasha la Nyangumi mwaka 2024 lililofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo.
Bw. Deodat Mmanda amesema vipo visiwa viwili ambavyo bado havijapata wawekezaji kutokana na changamoto mbalimbali za kuwekeza kwenye visiwa hivyo ikiwemo sababu za kiusalama hali inayorudisha nyuma uwekezaji.
Ameongeza kuwa MPRU wako tayari kuimarisha miundombinu na kutatua changamoto ambazo zikifanyiwa kazi maeneo hayo yatakuwa bora zaidi na kuwahamasisha wananchi na taasisi mbalimbali kujenga utamaduni wa kutembelea maeneo hayo ya hifadhi ili kuwavutia wageni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara imeombwa kutoa ushirikiano, ufafanuzi na elimu kwa wawekezaji wa vivutio vya utalii hasa kwenye maeneo ya fukwe ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza hususan za kiusalama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi ambae pia ni Mgeni rasmi wa tukio hilo amesema wizara hiyo iko kwenye mpango wa kutembelea Mkoa wa Mtwara na Lindi ili kuhakikisha vivutio vyote vilivyopo kwenye mikoa hiyo vinaingia kwenye mpango wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuvitangaza na kuviendeleza hivyo kuwataka viongozi wa mikoa hiyo kutoa ushirikiano ili kuandaa mpango wa kuendeleza vivutio vilivyopo.
"Lengo la Serikali na maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi mwaka 2025/2026 kuhakikisha kuwa wanafikia watalii milioni 5 hivyo ujio wa Nyangumi Festival 2024 utaongeza aina nyingine ya utalii na kuongeza idada ya watalii" alisema Dkt. Kohi.