MKAKATI WA KUKUZA UTALII KISIWA CHA MAFIA.
Tarehe Iliyochapishwa: Ijumaa, Juni 23, 2023
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii ( TTB) Ndugu Damas Mfugale,amekutana na Watumishi wa Hifadhi ya Bahari Mafia na kufanya kikao na Wadau wa Utalii katika Wilaya ya Mafia.Katika kikao hicho,Wadau wamefikisha maoni Yao kuhusiana na changamoto zinazokabili shughuli ya Utalii katika Kisiwa Cha Mafia na pia kuhusiana na aina ya Utalii ambayo wanatamani ufanyike Mafia. Baadhi ya changamoto zilizowasilishwa ni pamoja na kutokuwepo Kwa mpango wa pamoja wa kutangaza utalii wa Mafia hivyo kufanya Kila mdau ajitangaze Kwa uwezo binafsi,suala la kuongeza nguvu kwenye uhifadhi pia lilisisitizwa na Wadau hao Ili kuwezesha uendelevu wa rasilimali zinazovutia Watalii. Pamoja na changamoto mbalimbali zilizojadilwa pia wadau walitoa mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB) inaitazama Mafia kama sehemu muhimu ya Utalii wa Bahari. Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Kwa upande wake aliahidi kuhakikisha wanaweka nguvu zaidi kwenye kuitangaza Mafia kwenye Soko la Utalii lakini pia Kwa kuhakikisha pamoja na kutangaza panakuwa na Master Plan ya Kisiwa Cha Mafia Ili kuwa na utaratibu mzuri wa uwekezaji katika Utalii Ili kuepuka kuwa na Utalii holela na unao haribu mazingira. Kikao hiki ambacho kiliongozwa na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Mafia,katika kuhitimisha alisisitiza sana suala la uhifadhi na ushirikiano wa pamoja wa Wadau Wote wa Utalii. Halikadhalika alisema tayari Wilaya Kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mafia wameandaa Mpango wa Bajeti Kwa ajili ya kutengeneza Master Plan kiasi Cha shilingi bilioni 7 Kwa mwaka wa fedha unaokuja. Pia alitoa taarifa ya kufanyika Kwa Tamasha la Utalii la Mafia ( Mafia Tourism Festival) mnamo mwezi Agosti 2023 na kuwaomba Wadau wote wawe na utayari wa kushiriki mara mchakato wa maandalizi utakapoanza. Kwa pamoja Wadau wa Utalii Mafia wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Salum wamepanga kuwa na mjadala wa pamoja wa kujadili aina ya Utalii unaohitajika kufanyika Mafia. Wadau wa Utalii Mafia Kwa nyakati tofauti wamezungumzia furaha yao Kwa kuona uwepo wa mwanga mzuri wa kufunguka zaidi Kwa shughuli za Utalii.