SEKTA YA UVUVI KUPITIA UCHUMI WA BULUU KUPATIWA DOLA MILIONI 118 MKUTANO WA COP29
Benki ya Dunia (WB) kwa kushirikiana na Kampuni ya Nice Consulting Tanzania (LTD) wakiwa kama wadau wa maendeleo wameahidi kutoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 118 (Benki ya Dunia Milion 117 na NICE Dola Milion 1) kwa ajili ya kusaidia Sekta ya Uvuvi katika uchumi wa Buluu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe alishiriki katika Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCC - COP-29) unaoendelea katika jiji la Baku nchini Azerbaijan.
Katibu Mkuu alihutubia katika Mkutano huo akitoa maelezo ya utangulizi wakati wa Mkutano wa pembezoni uliofanyika Novemba 15, 2024. Mkutano huo ulikuwa unahusu Uvuvi Endelevu na Uchumi wa Buluu ambao uliangazia fursa za uwekezaji katika Sekta ya Uvuvi na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Mkutano uliongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa niaba ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango.