RC TANGA ATAKA RASILIMALI ZA BAHARI ZILINDWE KWA MANUFAA YA VIUMBE HAI
RC TANGA ATAKA RASILIMALI ZA BAHARI ZILINDWE KWA MANUFAA YA VIUMBE HAI

Jumanne, 25 June 2024, Tanga.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Burian amawataka wadau wa sekta ya uvuvi na bahari kuzilinda rasilimali za  Bahari kwa manufaa ya viumbe hai na kufanya uvuvi wenye tija na faida bila kuleta madhara kwa viumbe hao.

Ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya wadau wa sekta ya uvuvi na bahari ijulikanayo kama “Coral Reef Rescue Initiative” (CRRI) kwa lengo la kujengewa uelewa juu umuhimu wa uhifadhi wa matumbawe. 

“Tuhakilishe tunasimamia, tunafuatilia ili basi itusaidie kiuchumi, kiutalii lakini vilevile katika siku zijazo ziweze kutusaidia katika utafiti wa dawa mbalimbali zinazoweza kupatikana” alisema Dkt. Batilda.

Naye, Mhifadhi Mfawidhi kutoka Hifadhi ya Bahari Tanga Silikanti, Bi. Magreth Mchome ameelezea namna mazalia ya samaki yanavyoharibika kutokana na uvuvi haramu.

“Kumekuwa na vitendo vingi vya uharibifu hii ni kutokana na uvuvi haramu kwa kutumia milipuko ambayo ni mabomu, uvuvi wa kutumia makokoro na nyavu nyingine ambazo zinakwenda kuvunja miamba hiyo”.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu kutoka Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) na Mratibu wa Mradi huo Bw. Godfrey Ngupula alieleza kuwa lengo la warsha hii ni kuwajengea uelewa juu ya umuhimu wa Bahari na kuwa na makubaliano ya pamoja ya kuweza kuhifadhi rasilimali za bahari.