MPRU YATANGAZA FURSA YA UWEKEZAJI WA UTALII WA BAHARI MAONESHO YA SITE
MPRU YATANGAZA FURSA YA UWEKEZAJI WA UTALII WA BAHARI MAONESHO YA  SITE

Alhamisi, 16 Octoba 2024, Dar es Salaam

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imeshiriki kwa mafanikio katika Maonesho ya Nane ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo (SITE) yaliyofanyika kuanzia Oktoba 11-13, 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi. SITE, ambalo hufanyika kila mwaka, yanajikita katika kukuza safari za ndani na nje ya Afrika, likilenga kuvutia wadau wa utalii na usafiri kutoka kote ulimwenguni.

Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa "Tembelea Tanzania kwa Uwekezaji Endelevu na Utalii Usiomithirika," ikiwakutanisha waoneshaji takribani 120 wa bidhaa na huduma za utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania, na kuwezesha kuunganisha kampuni kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na Kati na kampuni za utalii za kimataifa.

MPRU ilitumia fursa hii kutangaza fursa za kipekee za uwekezaji katika utalii wa bahari kupitia kauli mbiu “Where Investment Meets Marine Exploration.” Kwa kushiriki katika majukwaa mbalimbali na mijadala wakati wa maonesho hayo, MPRU ililenga kuunganishwa na wawekezaji na wanunuzi wa bidhaa za utalii, na kutangaza uwezekano wa utalii wa bahari ndani ya maeneo yake yaliyohifadhiwa.

Aidha, MPRU iliandaa vikao kadhaa katika banda lake la maonesho (G02) vilivyowezesha mikutano na wanunuzi pamoja na wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali.

Wageni waliotembelea banda la G02 walipata nafasi ya kujifunza kuhusu juhudi za MPRU, ikiwemo visiwa vinavyosimamiwa na taasisi hiyo, juhudi zake za uhifadhi wa bahari, na namna wanavyoshirikiana na jamii za maeneo hayo katika kulinda mifumo ya ikolojia ya bahari.

Wageni pia waliopata kufika katika banda la MPRU walifahamishwa jinsi ya kufika kwenye visiwa hivyo, shughuli za kitalii zinazopatikana, pamoja na aina mbalimbali za viumbe wa baharini na vivutio vinavyofanya maeneo hayo kuwa ya kipekee.

Kupitia ushiriki wake katika SITE, MPRU inalenga kupanua soko la utalii wa bahari pamoja na uhifadhi, ili kuchangia kwenye uchumi wa buluu kwa kukuza matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Aidha, katika juhudi za kuimarisha mitandao na mahusiano katika sekta ya uhifadhi na utalii wa bahari, MPRU inaendelea kuhamasisha na kufahamisha umma juu ya fursa za uwekezaji endelevu na uchunguzi wa kipekee ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa ya bahari ya Tanzania.