MPRU, e-GA WASHIRIKIANA MAFUNZO YA MFUMO MPYA WA MTANDAO
Tarehe Iliyochapishwa: Jumatano, Novemba 22, 2023
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ikiongozwa na wataalam wake wameendesha mafunzo ya Mfumo wa kidigitali ujulikanao kama e-Mrejesho kwa watumishi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU).
Kupitia mfumo huo wa e-Mrejesho utamuwezesha mwananchi kuwasilisha malalamiko, kero, maoni, mapendekezo, au maulizo moja kwa moja kuhusiana na MPRU sambamba na kufuatilia utekelezaji wake.
Aidha, mfumo huo wa kidigitali una lengo la kumsaidia mwananchi kupunguza gharama pamoja na kuokoa muda wa kutembea umbali mrefu ili kuwasilisha maoni, mapendekezo au kufuatilia malalamiko yake.
Sanjari na hayo, mfumo huu wa e-Mrejesho utatoa fursa kwa MPRU kupitia maoni ya aina tofauti katika kuimarisha huduma kwa upande wa Visiwani na katika shughuli nzima za utalii wa Bahari katika kufikia malengo waliyojiwekea.
Mfumo wa e-mrejesho unapatikana katika tovuti ya www.emrejesho.go.tz, au kwa kupakua ‘application’ ya eMrejesho kwa kutumia simu janja au kupiga namba ya msimbo *152*00# kisha chagua namba 9, kisha chagua 2 na kisha fuata maelekezo.