MFUMO WA e-CAS WATUMIKA KUBAINI TAKWIMU ZA SAMAKI WALIOKAMATWA MIMP
Jumanne, 17 Julai 2024, Mafia
Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP) wameendesha warsha ya kupokea ripoti ya maoni kuhusu takwimu zilizokusanywa kwa kutumia mfumo wa Serikali ujulikanalo kama e-CAS kubaini samaki waliokamatwa ndani ya Kisiwa cha Mafia.
Warsha hiyo ilifunguliwa na Mhifadhi Mfawidhi kutoka MIMP, Bw. Amin Abdallah ambaye alisisitiza umuhimu wa takwimu katika kusimamia Hifadhi na mikakati ya uhifadhi. Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Mfuko wa Shughuli za Bluu (BAF) kwa kushirikiana na ‘World Wildlife Fund’ (WWF).
Wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) waliwasilisha matokeo ya ukusanyaji wa takwimu na matokeo yanayoangazia hali ya samaki ndani ya MIMP. Warsha hiyo ilihudhuriwa na Timu ya Watumishi wa MIMP, Kamati ya Uhifadhi (VLC) pamoja na Afisa wa Uvuvi.