MENEJA MPRU AHIMIZA USHIRIKIANO KATIKA UHIFADHI NA UTALII WA BAHARI MTWARA
Jumatano, Aprili 01, 2026, Mtwara
Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU), Dkt. Emmanuel Sweke, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kituo cha Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma (MBREMP) mkoani Mtwara Aprili 01, 2026.
Katika ziara hiyo, Dkt. Sweke alikutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) Mtwara, Bw. John Tilubuzya, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mh. Abdallah Mwaipaya, pamoja na Afisa wa Usimamizi wa Bahari na Ikolojia kutoka Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) Mtwara, Bw. Said Shaib.
Akizungumza katika mazungumzo hayo, Dkt. Sweke alijitambulisha kwa wadau hao na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika juhudi za kuhifadhi na kutumia kwa uendelevu rasilimali za bahari na kubainisha kuwa juhudi hizo pia zinahusisha kukuza utalii wa bahari, hususan utalii wa Nyangumi katika eneo la Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma (MBREMP).
Aidha, Dkt. Sweke alieleza kuwa kila mwaka kuanzia mwezi Julai hadi Novemba, eneo la MBREMP hupokea Nyangumi aina ya Humpback Whale wanaohama kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto wao, tukio linalotoa fursa ya kipekee ya utalii wa baharini. Kutokana na umuhimu huo, MBREMP kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huandaa maonesho yanayojulikana kama Mnazi Bay Nyangumi Festival ambapo Maonesho hayo hufanyika wakati wa Kilele cha Msimu wa Nyangumi, kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi na kutangaza vivutio vya utalii wa bahari.
Katika hatua nyingine, Dkt. Sweke alitembelea Kisiwa cha Namponda kilichopo ndani ya MBREMP, ambapo alipata fursa ya kujionea hali ya uhifadhi pamoja na mandhari ya kisiwa hicho. Aidha, alifanya kikao na watumishi wa MBREMP, kusikiliza maoni, ushauri na changamoto zinazowakabili, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

