MBREMP YAWAKARIBISHA WADAU WA UHIFADHI KATIKA TAMASHA LA NYANGUMI FESTIVAL 2024
Ijumaa, 23 Agosti 2024, Mtwara
Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma inawakaribisha wadau wa uhifadhi kushiriki katika maonesho ya tamasha la Nyangumi Festival 2024 linalotarajiwa kufanyika katika maeneo mawili tofauti moja ni katika viwanja vya Mashujaa pamoja na Kituo cha Ghuba ya Mnazi (Manzi Bay) vyote vilivyopo Mkoani Mtwara.
Kupitia mahojiano aliyofanya na chombo cha habari cha Mtwara online tv, Mhifadhi Mfawidhi kutoka MBREMP Dkt. Reidfred Ngowo alithibitisha uwepo wa tamasha hilo la Nyangumi Festival 2024 na kuwakaribisha wadau wa uhifadhi kuja kushiriki katika tamasha hilo.
“Napenda kuwataarifu wadau wetu wote wa uhifadhi tutakuwa na tamasha kubwa la nyangumi ambapo tamasha hili litafanyika sehemu mbili katika viwanja vya mashujaa pamoja na mnazi bay” alisema Dkt. Ngowo.
Aidha, Dkt. Ngowo alieleza kupitia tamasha hilo washiriki watapata fursa ya kuona maonesho ya bidhaa mbalimbali, maonesho ya uhifadhi kutoka taasisi mbalimbali kutoka Kusini mwa Tanzania.
Halikadhalilika, katika kusherehesha tamasha hilo kutakuwa na shughuli za burudani na michezo mbalimbali iliyoandaliwa kama kivutio kwa washiriki na nafasi ya kuweza kuweka utimamu wa mwili sawa kupitia michezo mbalimbali iliyoandaliwa katika tamasha hilo.
“Kutakuwa na ngoma na burudani za aina mbalimbali na hiyo itaenda sambamba kila siku kwa wale waliojiandikisha watapata nafasi ya kwenda Mnazi Bay ambapo kule wataenda kutembelea Nyangumi, michezo ya beach itakayokuwa inafanyika pamoja na burudani mbalimbali, huduma ya vinywaji, samaki choma nakadhalika.
Aidha, Dkt. Ngowo alithibisha ushiriki wa wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mtwara pamoja na nje ya nchi ambao watashiriki tamasha la Nyangumi Festival 2024.
Nyangumi wamekuwa kivutio kwa watu ndani na nje ya nchi kwa kuwa wanyama hao wamekuwa na sifa za kipekee ambazo ni pamoja na kuwa ni viumbe wakubwa wanaoishi majini wakiwa na uzito mkubwa unakadiriwa kufika tani 40,000.
Nyangumi hubeba mimba kwa kipindi cha miezi 12 na mtoto wake huzaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 900 hadi 1000, akiwa na uwezo wa kuzaa kila baada ya miaka mitatu.
Tamasha la Nyangumi Festival 2024 linatarajia kufanyika Agosti28, 2024.