HESHIMU BAHARI YAWEZESHA MENEJIMENTI MPRU KUPATA MAFUNZO
Jumanne, 10 Septemba 2024, Tanga
Menejimenti ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imefanya mafunzo ya siku tano (5), yaliyoanza Jumatatu tarehe 2-6 Septemba, 2024 mkoani Tanga. Mafunzo haya yanatolewa kwa ushirikiano wa programu ya mradi wa miaka mitano (5) wa Heshimu Bahari (Respect Ocean) kwa hisani ya watu wa Marekani USAID.
Mafunzo haya yanalenga kuimarisha uwezo wa timu ya menejimenti ya MPRU katika nyanja za uongozi, usimamizi (adaptative Management), mikakati ya usimamizi yenye ufanisi, kutatua migogoro, na usimamizi shirikishi. Erin Barlow na Eliezeri Sungusia kutoka DOI ITAP wanatoa mafunzo haya, yakilenga kuongeza ushirikiano na mawasiliano katika Nyanja za Uongozi ili MPRU iweze kufikia malengo yake ya kulinda asilimia 30 ya hifadhi zake ifikapo mwaka 2030.
Meneja wa MPRU, Bw. Davis Mpotwa ameishukuru Menejimenti ya MPRU pamoja na wawezeshaji wa mafunzo hayo katika ushiriki wao wa mafunzo hayo kwani yanachangia pakubwa katika kufanikisha dhamira ya taasisi.
“Asanteni kwa kushiriki katika mafunzo haya, uthabiti wenu katika kujifunza na uongozi unachangia pakubwa katika maendeleo na kufanikisha dhamira yetu. Mikakati na maarifa tuliyopata yatasaidia kuongeza ufanisi wa Taasisi katika kutekeleza majukumu yake” alisema Mpotwa.
Bw. Mpotwa aliwataka washiriki mafunzo hayo watumie elimu hiyo kwa ufanisi kwa kuendelea kuleta athari chanya kwa bahari na jamii kwa ujumla. “Tuitumie mafunzo haya kwa ufanisi na tuendelee kuleta athari chanya kwa bahari yetu na jamii zetu”, alieleza Mpotwa. Aidha, aliendelea kwa kutoa rai kwa Heshimu Bahari na wadau wengine kuendelea kushirikiana katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari kwa matumizi endelezo.
Halikadhalika, Bw. Mpotwa alitumia nafasi hii kuitambulisha Tuzo aliyokabidhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya Taasisi hiyo kushika nafasi ya pili kati ya Taasisi 253 katika kipengele cha "Operational Excellence and Financial Performance."