DC RUFIJI AWATAKA WANANCHI KUTUNZA MATUMBAWE
DC RUFIJI AWATAKA WANANCHI KUTUNZA MATUMBAWE

Ijumaa, 1 Machi 2024, Pwani

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amewataka Wananchi hususani wanaojishughulisha na Uvuvi pamoja na mazao ya bahari kuacha kuharibu miamba ya makuzi ya vizalia vya viumbe hai Wanaoishi baharini (Matumbawe) ili kutunza uhai wa viumbe hivyo.

Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya namna ya uhifadhi wa miamba ya makuzi ya vizalia vya viumbe hai wanaoishi baharini yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri  uliopo Wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

“Niombe wadau mlioshiriki hapa leo ndo maana tumejumuisha na wavuvi, tusipotunza maana yake kesho hatutauza na hatutazalisha kwa sababu sisi tunajua nani anavua kwa kutumia uvuvi haramu mfano wa baruti, kwahiyo tukawe wakali vinginevyo tutapoteza hizi spicies (viumbe hai) katika maeneo yetu” Alisisitiza Meja Gowele

Akielezea faida ya miamba hiyo baharini Mhifadhi Mkuu wa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu, Bw. Godfrey Ngupula amesema miamba hiyo ndio uhai wa viumbe hai wanaoishi baharini na kufafanua kuwa kutokuwepo kwa miamba hiyo itasababisha viumbe hao kukosa makazi maalumu ya kuzaliana na kutunza viumbe baharini ambapo moja ya jambo linaloweza kusababisha kuvunjika kwa miamba hiyo ni ukataji holela wa miti ya mikoko pembezoni mwa bahari.

"Matumbawe ni eneo dogo sana halizidi hata asilimia moja ya bahari yote, zaidi ya asilimia 80 ya Wavuvi wa kawaida wanategemea uhai wa matumbawe, kwahiyo Matumbawe ni miamba iliyopo baharini. Sasa kwenye ufukwe huku kua Matumbawe mengi sana ni zaidi ya upana wa km 1 mpaka 3 lakini pia ni marefu kuanzia Mtwara, Kilwa, Mafia, Kibiti, Rufiji (Mohoro), Tanga na Pemba. Sasa rasilimali hii lazima itunzwe” amesisitiza Ngupula.