DC MTWARA AWATAKA WAKAZI WA MTWARA KUFANYA UTALII WA NDANI
DC MTWARA AWATAKA WAKAZI WA MTWARA KUFANYA UTALII WA NDANI

Jumanne, 3 Septemba 2024, Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Mwanahamisi Munkunda amewataka wakazi wa Mkoa wa Mtwara kufanya utalii wa ndani kwani Mkoa huo una vivutio vingi vya utalii ambavyo bado havijulikani miongoni mwa watu wengi.

Ameyasema hayo alipokuwa akizindua rasmi Tamasha la Nyangumi 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambapo uzinduzi wa tamasha hilo ulifanyika Agosti 28, 2024 katika viwanja vya Mashujaa.

“Mtwara una vivutio vingi vya kiutalii ambavyo bado havijulikani kwa watu, ni kiu ya Mhe. Rais Samia kuona Mkoa wa Mtwara unafunguka kiutalii na kiuchumi; tayari tumeanza kutumia bandari ya Mtwara kusafirisha mazao ya korosho sasa tutangaze vivutio vyetu ikiwemo Msimu huu wa Nyangumi 2024 ili wageni waje lakini pia na sisi wakazi twende tukafanye utalii wa ndani” alieleza Mhe. Munkunda.

Halikadhalika, Mhifadhi Mfawidhi kutoka Hifadhi ya Bahari Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma, Dkt. Reidfred Ngowo akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo alisema Nyangumi huonekana katika Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma kuanzia mwezi Julai mpaka Novemba kila mwaka kwani mazingira hayo ni rafiki kwao kwa kukidhi mahitaji yao ya kujamiiana, kuzaana na kulea.

“Nyangumi wamekuwa kivutio kwa watu ndani na nje ya nchi kwa kuwa wana sifa za kipekee ikiwa ni pamoja na kuwa ni viumbe wakubwa wanaoishi majini wakiwa na uzito unakadiriwa kufikia tani 40 lakini pia Nyangumi hubeba mimba kwa kipindi cha miezi 12 na mtoto wake huzaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 900 hadi 1000 huku akiwa na uwezo wa kuzaa kila baada ya miaka mitatu” alieleza Dkt. Ngowo

Tamasha hilo limelenga kujenga uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali ambazo zinahifadhiwa na kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga hoteli.

Naye wa upande wake, Mhifadhi wa Bahari, Mussa Ally ameitaka jamii ya wavuvi kutowavua Nyangumi kwani husaidia kunyonya hewa ya ukaa ambayo inaleta athari kubwa.

Aidha, maonesho hayo yanaendelea katika viwanja vya Mashujaa mpaka tarehe 06/09/2024 ambapo wananchi watapata fursa ya kujiandikisha kwaajili ya kwenda Msimbati maadhimisho ya kilele cha Tamasha la Nyangumi tarehe 07/09/2024.