MATUMBAWE NI KIVUTIO KIKUBWA CHA WATALII - DC KILWA
MATUMBAWE NI KIVUTIO KIKUBWA CHA WATALII - DC KILWA

Tarehe Iliyochapishwa: Jumatatu, Januari 29, 2024

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Christopher Ngubiagai amesema kuwa matumbawe ni moja ya kıvutio kikubwa cha watalii nchini na kuelezea umuhimu wake katika kukuza kipato kwa wananchi.

Mhe. Ngubiagai aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika warsha ya “National Working Group” iliyofanyika Wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi Januari 26, 2024.

“Matumbawe ni kivutio cha watalii tunaweza kuitangaza Kilwa yetu hasa tukiwa na matumbawe ya kutosha na kupata mapato makubwa yanayotokana na watalii wengi kutembelea Kilwa yetu nasi tunapokuwa na matumbawe ya aina mbalimbali” alisema Mhe. Ngubiagai.

"Matumbawe yana umuhimu mkubwa katika maisha ya binadamu ikiwemo kukuza pato la wananchi haswa wananchi wanaoishi katika ukanda wa Pwani kwavile kukosekana kwake kunasababisha adha kubwa ya kupotea kwa samaki na bahari inakuwa sio sehemu ya Uchumi wa Buluu" aliongezea Mhe. Ngubiagai.

Aidha, Mhe. Ngubiagai ameishukuru Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) kwa mualiko wa ushiriki katika mradi wa “Coral Reef Rescue” uliofanyika katika Wilaya hiyo ukiongozwa na mratibu wa mradi huo, Bw. Godfrey Ngupula, Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi (MPRU).